1 Samuel 15

Bwana Anamkataa Sauli Asiwe Mfalme

1 aSamweli akamwambia Sauli, “Mimi ndiye ambaye Bwana alinituma nikutie mafuta uwe mfalme juu ya watu wake Israeli, basi sasa sikiliza ujumbe kutoka kwa Bwana. 2 bHili ndilo Bwana Mwenye Nguvu Zote asemalo: ‘Nitawaadhibu Waamaleki kwa kile walichowatendea Israeli walipowavizia wakati walipanda kutoka Misri. 3 cBasi sasa nenda ukawashambulie Waamaleki na kuwaangamiza kabisa pamoja na kila kitu kilicho mali yao. Usiwahurumie; waue wanaume na wanawake, watoto na wanyonyao, ng’ombe na kondoo, ngamia na punda.’ ”

4 dNdipo Sauli akawaita watu na kuwapanga huko Telaimu, askari wa miguu 200,000 pamoja na watu 10,000 kutoka Yuda. 5Sauli akaenda katika mji wa Amaleki na kuwavizia bondeni. 6 eKisha akawaambia Wakeni, “Ondokeni, waacheni Waamaleki ili nisije nikawaangamiza ninyi pamoja nao, kwa kuwa ninyi mliwatendea mema Waisraeli wote wakati walipanda kutoka Misri.” Basi Wakeni wakaondoka, wakawaacha Waamaleki.

7 fNdipo Sauli akawashambulia Waamaleki toka Havila mpaka Shuri, hadi mashariki ya Misri. 8 gAkamchukua Agagi, mfalme wa Waamaleki akiwa hai, nao watu wake wote akawaangamiza kabisa kwa upanga. 9 hLakini Sauli na hilo jeshi wakamhifadhi hai Agagi na kondoo na ng’ombe walio wazuri, mafahali na wana-kondoo walionona kila kitu kilichokuwa kizuri. Hivi vitu hawakuwa radhi kuviangamiza kabisa, bali kila kitu kilichodharauliwa na kilicho dhaifu wakakiangamiza kabisa.

10Kisha neno la Bwana likamjia Samweli kusema: 11 i“Ninasikitika kwamba nimemfanya Sauli kuwa mfalme, kwa sababu ameacha kunifuata mimi na hakutimiza maagizo yangu.” Samweli akafadhaika, naye akamlilia Bwana usiku ule wote.

12 jAsubuhi na mapema Samweli akaamka kwenda kukutana na Sauli, lakini akaambiwa, “Sauli amekwenda Karmeli. Huko amesimamisha mnara kwa heshima yake mwenyewe naye ameendelea na kuteremkia Gilgali.”

13 kSamweli alipomfikia, Sauli akamwambia, “Bwana akubariki! Nimetimiza yale Bwana aliniagiza.”

14Lakini Samweli akasema, “Nini basi huu mlio wa kondoo masikioni mwangu? Huu mlio wa ng’ombe ninaousikia ni kitu gani?”

15 lSauli akajibu, “Askari wamewaleta kutoka kwa Waamaleki, waliwaacha wale kondoo na ng’ombe wazuri ili kuwatoa dhabihu kwa Bwana, Mungu wako, lakini tuliwaangamiza kabisa wengine wote.”

16Samweli akamwambia Sauli, “Ngoja! Nami nitakuambia lile Bwana aliloniambia usiku huu.”

Sauli akajibu, “Niambie.”

17 mSamweli akamwambia, “Ingawa zamani ulijiona mdogo machoni pako mwenyewe, Je, hukuwa kiongozi wa kabila za Israeli? Bwana alikutia mafuta kuwa mfalme juu ya Israeli. 18Naye akakutuma kwa kazi maalum, akisema, ‘Nenda ukaangamize kabisa wale watu waovu, wale Waamaleki, upigane nao vita mpaka utakapowaangamiza kabisa.’ 19 nKwa nini hukumtii Bwana? Kwa nini ulivamia nyara na kufanya uovu machoni pa Bwana?”

20 oSauli akasema, “Lakini nilimtii Bwana. Nilikamilisha ile kazi ambayo Bwana alinituma. Niliwaangamiza Waamaleki kabisa na kumleta Agagi mfalme wao. 21Askari walichukua kondoo na ng’ombe kutoka kwenye nyara, zile ambazo ni nzuri sana zimewekwa wakfu kwa Mungu, ili zitolewe dhabihu kwa Bwana Mwenyezi Mungu wako huko Gilgali.”

22 pLakini Samweli akajibu: “Je, Bwana anafurahia sadaka za kuteketezwa na dhabihu
kama vile kuitii sauti ya Bwana?
Kutii ni bora zaidi kuliko dhabihu,
nako kusikia ni bora
kuliko mafuta ya kondoo dume.

23 qKwa maana kuasi ni kama dhambi ya uaguzi,
nao ukaidi ni kama uovu wa kuabudu sanamu.
Kwa sababu umelikataa neno la Bwana,
naye amekukataa wewe
kuendelea kuwa mfalme.”

24 rNdipo Sauli akamwambia Samweli, “Nimetenda dhambi. Nimevunja amri ya Bwana na maagizo yako. Niliwaogopa watu na kwa hiyo nikafanya walivyotaka. 25 sSasa ninakusihi usamehe dhambi yangu, nawe urudi pamoja nami, ili nipate kumwabudu Bwana.”

26 tLakini Samweli akamwambia, “Sitarudi pamoja nawe. Umelikataa neno la Bwana, naye Bwana amekukataa wewe, usiendelee kuwa mfalme juu ya Israeli!”

27 uSamweli alipogeuka ili aondoke, Sauli akang’ang’ania pindo la joho lake, nalo likararuka. 28 vSamweli akamwambia, “Bwana ameurarua ufalme wa Israeli kutoka kwako leo, naye ameutia kwa mmoja wa majirani zako, aliye bora kuliko wewe. 29 wYeye aliye Utukufu wa Israeli hasemi uongo wala hana kigeugeu; kwa kuwa yeye si mwanadamu, hata abadili nia yake.”

30 xSauli akajibu, “Nimetenda dhambi. Lakini tafadhali niheshimu mbele ya wazee wa watu wangu na mbele ya Israeli; rudi pamoja nami, ili nipate kumwabudu Bwana Mwenyezi Mungu wako.” 31Hivyo Samweli akarudi pamoja na Sauli, naye Sauli akamwabudu Bwana.

32Ndipo Samweli akasema, “Niletee Agagi mfalme wa Waamaleki.”

Agagi akaja kwake kwa ujasiri, akifikiri, “Hakika uchungu wa mauti umepita.”

33 yLakini Samweli akasema, “Kama upanga wako ulivyofanya wanawake
kufiwa na watoto wao,
ndivyo mama yako atakavyokuwa
hana mtoto miongoni mwa wanawake.”

Naye Samweli akamuua Agagi mbele za Bwana huko Gilgali.

34 zKisha Samweli akaenda Rama, lakini Sauli akapanda nyumbani kwake huko Gibea ya Sauli. 35 aaHadi siku Samweli alipofariki hakwenda kumwona Sauli tena, ingawa Samweli alimwombolezea. Naye Bwana alihuzunika kwamba alimfanya Sauli kuwa mfalme juu ya Israeli.
Copyright information for SwhKC